Ukurasa wa mbele
Gazeti la injili
Nyimbo za Munishi
Soma barua Yahoo
Soma barua Hotmail
Tuma SMS duniani
Sema nami
Sikiliza waongo
Twende kanisani
Gazeti INJILI http://munishi.netfirms.com
E-mail: munishifaustin@yahoo.com
Or fmunishi@hotmail.com

Majambazi Wamvamia Munishi Nyumbani

 

Genge la majambazi wenye silaha walimvamia Mwinjilisti na mwimbaji wa nyimbo za injili Faustin Munishi nyumbani kwake huko Ngong Oloolua usiku wa kuamkia leo tarehe 24.10.2001. Wezi hao ambao idadi yao inakisiwa kuwa kumi walikata dirisha wakitumia mkasi wa chuma kisha wakaingilia dirishani na kutumia jiwe kubwa kuvunja milango ya vyumbani.

Zoezi hilo lililochukua zaidi ya nusu saa lilimwacha Munishi bila video recorder mbili ambazo thamani yake ni Kshs.26,000, Video kamera moja ya Ksh.65000, Tv seti moja Ksh. 14000, Setilaiti Receiver moja Ksh 80,000 Video Sender yenye uwezo wa kurusha matangazo ya TV umbali wa kilometa moja mraba Ksh 30,000 Simu mbili za mkononi Nokia 3210 na Seamens zote Ksh.20,000 Pamoja na vito vya dhahabu ikiwemo pete ya ndoa Ksh 20,000.

Akiongea akiwa mtulivu Munishi alisema, ''Namshukuru Mungu kwani aliwatuliza majambazi na hawakumdhuru yeyote nyumbani.''Waliingia saa saba na nusu usiku, niliwasikia wakikata dirisha la sebuleni, na nikamwita mke wangu ambaye alianza kupiga mayowe ambayo yalikatizwa na kishindo kikubwa cha jiwe liliogonga mlango wa chumba chetu. Tulichokiona ni mwanga mkali wa tochi na sauti ya ukali ikituamuru tulale chini na tunyamaze.

Walianza kupekua kila mahali chumbani hapo na baadaye walinitaka niwape pesa. Niliwaelekeza mahali kulipokuwa pochi yangu ambayo ilikuwa na Ksh.1,500 tu. ''Baada ya kuzichukua shilingi 1500 ambazo ndizo pekee nilizokuwa nazo, walinitaka niwape pesa nyingine na nilipowaambia kuwa sina. Ilionekana kama walinielewa na kuniamini jambo lililowafanya waanze kuchukua vitu ambavyo nimevifanyia kazi maisha yangu yote.

Baada ya wezi kuondoka ndipo tulipopiga mayowe na majirani wakatoka, lakini wezi walikuwa wameshaondoka dakika kumi zilizopita. Majirani walipiga simu 030340077 katika kituo cha polisi cha Ngong ambao walikuja baada ya dakika kumi.nawashukuru Polisi kwa kufika mapema, na nina matumaini kwamba vitu vyangu vitapatikana.

Kinachoniuma siyo vitu walivyochukua, bali ni swali aliloniuliza mtoto wangu mdogo wa miaka saba. "Baba kwa nini unanyamaza na kuwaacha wachukue vitu vyetu?" Sikumjibu na mpaka sasa sijamjibu na sijui kama nitaweza kumjibu akarithika.

"Sitaki kuunganisha kisa hiki cha majambazi na barua za matisho ambazo nimekuwa nikipokea siku tatu zilizopita, lakini pia sitaki kusema ni wizi wa kawaida maana sijui tofauti kati ya wizi wa kawaida na usio wa kawaida. Ukiwa umesoma makala yangu "WANASIASA NI WEZI WALIOINGILIA DIRISHANI NA WANATAKA WATOKEE MLANGONI halafu ulinganishe na wezi walioingia kwangu wakipitia dirishani na wakati wanatoka na vitu wakamwamuru mke wangu awape funguo za mlango ili watoke na vitu, hutakosa kuwanyooshea kidole wanasiasa.

"Juzi nilipata barua ya matisho ya E-Mail ...

Hi Munishi, whoever you are but get ready to defend the truth... Munishi, you have been in Kenya for along time right? You know nothing about tanzania considering your bad education background.. Look at this "Ninaujua ugumu wa kazi hiyo hasa ukitilia maanani kwamba Nyerere alitumia muda wote wa utawala wake kujikita katika nyoyo za watanzania ili wamkumbuke miaka 100 ijayo. Mwaka mmoja tangu afe kwa ugonjwa wa MKANDA WA JESHI{na sijui ni ugonjwa gani huo.}Tayari hisia za watu juu yake zimeanza kubadilika ghafla." It shows your ignorance if not stupidity of analyzing things... Hey, guess what, I thought you are Christian, you stated by your fake songs, don't you remember Munishi you were one one the Majambazi sugu?" Do you want us to make a followup and as one of the person you killed my relative during that time and I am convinced you are still jambazi sugu under the cover of christianity. We warn you to stop writing these stupid ideas about the late Nyerere, this man used to be the one who was making peace internationally and you cannot even compare any these stupid ideas and his. Yes, if you think he was wrong, who is right? I know you think Tanzanian will listen to you, but we will put your issue open Ok... GO ON>>>

Jana Tarehe 23.10.2001 nilisoma makala katika gazeti la NATION na nikatoa maoni yangu na kuyatuma katika baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo BBC, KTN, KBC na NATION

Sijui kama kuna chombo kilichotangaza maoni yangu, lakini waandishi wengi wa habari wana uhusiano wa karibu na wanasiasa.Makala iliyonifanya nitoe maoni ilikuwa na kichwa cha maneno
Moi must learn to let go

Baada ya kuyasoma kwa makini nilihisi mwandishi alikuwa na mengi yaliyotakiwa yaandikwe kwenye makala yake lakini kwa sababu ambazo anazijua mwenyewe hakuyaandika. Ndipo nilipoanza kwa kumuuliza swali.

Kwa nini Unazunguka Mbuyu? Sema liwalo na liwe.Kenya ni ya Wakenya na wao pekee ndio wanaostahili kuchagua nani awaongoze. Mambo ya kupigania uhuru yalipita na sasa ni mambo mapya. Kwamba mtu au jamii fulani ilihusika katika harakati za kupigania uhuru haimpi haki ya kuwaamulia nani aongoze nchi yenu.

Tanzania inaongozwa na Nyerere akiwa kaburini na Watanzania hawana cha kujivunia. Nyerere aliona Mkapa anatufaa watanzania na sisi tukakosea kumkubali bila kumuuliza maswali kwa heshima Kwamba Nyerere alipigania Uhuru. Wakenya msifanye makosa hayo. Mara nyingi hawa tunaofikiri kuwa wanaweza kututengenezea warithi, hata wao hawajui kilicho ndani ya mioyo ya hawa wanaodhaniwa kuwa wanaweza kuwarithi. Nyerere alimteua Mwinyi, na baadaye alimkemea kana kwamba alikuwa amekufa akafufuka na kumkuta Mwinyi akifanya mambo ya ajabu. Kumbe yeye mwenyewe ndiye aliyesema hakuna mtu aliyemfaa kama Mwinyi.

Ghaitho usifikiri nakupambanisha, lakini niliposoma kichwa cha makala yako Moi must learn to let go nilifikiri utatoboa jipu na ulikamue litoe usaa wote. Nasikitika kusema nilichokisoma ni mtu aliyekuwa akizunguka mbuyu makusudi ilihali anajua nini cha kufanya. Mimi sijasomea uandishi wa habari na pengine ndio sababu sijui kuuma na kupuliza. Ikiwa kusomea taaluma ya uandishi kutanifanya niume na kupuliza, basi nitabaki mwandishi wa jua kali ambaye nikiwa na sababu za kutosha kuuma nauma hasa.

Sijui unaogopa nini? Nitakuja hapo Nation uninong'oneze. Unawaogopa Wanasiasa? Hujui kwamba Wanasiasa ni wezi wanaotaka walindwe na sheria, ileile waliyoivunja wakiingia madarakani. Waliingia isivyo halali, wanataka watolewe kihalali. Walipitia dirishani, wanataka kutokea mlangoni. Hawaoni haya kuitumia sheria wasiyoitii iwasaidie kuwaweka kizuizini wote wanaowataka watoke madarakani kama walivyoingia.

Wanasahau sheria ni Msumeno unaokata kuwili. Wanataka sheria iwazuie wengine wasiibe, lakini waibe wao. Mwisho wao umefika, wametuibia vya kutosha. Sasa tunataka mapinduzi ya kuwatoa wezi kama walivyoingia. Ikiwa waliingilia dirishani wakiwa wembamba, watatokea hapo hapo baada ya kunenepa kwa mali za wizi. Wananchi tumeanza mapambano ambayo hayatanyamazishwa na mtutu wa bunduki, bali haki kwa kila binadamu itakapotendeka, ndipo vita yetu itakoma.

Wanatumia sheria walizozitunga wenyewe wakashindwa kuzitii, sisi tutatumia sheria za Mungu atupaye uwezo wa kuzitii. Kinyume na sheria za wanadamu zilizo na upungufu, sheria za Mungu ni kamili. Yeye hana upendeleo kwa mtu awaye yote. Mungu alisema tuzitii mamlaka, lakini zile tu zinazotoka kwake. Torati na manabii wote walikuwa kinyume na mamlaka dhalimu, sioni kwa nini sisi tunaohubiri Injili ya Yesu Mwokozi tukubaliane na udhalimu huu.

Yesu mwenyewe aliwaita wanasiasa mbweha sioni sababu ya sisi kuwaita waheshimiwa. Wanaheshimiwa kwa nini? Eti walianzisha taifa? Mungu ndio mwanzo wa kila kitu. Eti walitutoa katika minyororo ya wakoloni? Ni nini ikiwa walipotutoa minyororo walitufunga ya kwao? Wanasema walitujengea vituo vya afya? Mbona havina dawa? na zile zilizoko mwananchi hawezi kumudu gharama zake? Mbaya zaidi wao wenyewe hawatibiwi huko.

Lakini Mungu hana upendeleo, kwani anahakikisha kuwa wanasiasa wanapokwenda ngambo wakiwa moto kutafuta huduma nzuri za kiafya, wanarudi wakiwa baridi pamoja na juhudi zote za kujaribu kuyaokoa maisha yao. Na wananchi walioachwa na zahanati ambazo hazina dawa, Mungu anahakikisha kuwa chochote watakachokitumia kama dawa kinawatibu na wanapona kabisa, ili Mungu abaki kuwa Mungu, na wanasiasa wabaki kuwa wanadamu waongo.

Kuna uvumi kuwa siasa duniani zinaendeshwa na makundi ya watu waovu ambao hutegemea mapato haramu kutoka katika biashara ya madawa ya kulevya, pamoja na magendo ya kila aina. Ni makundi hayo ndiyo yanayoamua nani awe kiongozi wapi ili mradi maslahi yao haramu yalindwe. Wanatumia mabilioni ya pesa kushinikiza chaguzi zote duniani. Wanaoshinda uchaguzi siyo wale wanaopendwa na wananchi wa nchi husika, bali ni wale ambao sera zao zinalinda maslahi ya majambazi hao wa kimataifa.

CCM chama kinachotawala Tanzania kwa sasa, siyo kwamba kinapendwa na umma wa Watanzania, bali ni chama cha majambazi wa Tanzania kilichofadhiliwa na wenzao wa kimataifa ili kulinda maslahi yao. Ndio maana tunasema kwa ujasiri kuwa siasa ni uongo na dunia haifai kuongozwa kisiasa. Dunia ni ya Mungu, na inafaa kuongozwa kidini. Na huu ndio wakati unaofaa kufanya mageuzi hayo.

Wanasiasa pamoja na waandishi wa habari wanaojiita Third Estate, wameshirikiana kuifikisha dunia mahali ilipo. Sasa ni wakati wetu watumishi wa Mungu au kama tunavyojulikana First Estate, kuiokoa dunia isiangamie.

Usisahau Kenya ni ya Wakenya kama ilivyo Tanzania ni Ya Watanzania

Nchi ya Tanzania ni mali ya watanzania wote na siyo ya Mkapa na CCM kama inavyoekea kuwa.Vitendo vinavyofanywa na serikali ya chama tawala CCM vinaonyesha wazi jinsi wanavyofikiri kuwa Tanzania ni mali yao. Kwamba serikali inaweza kuwaua raia wake kwa sababu wana mawazo yanayotofautiana na chama tawala, siyo tu ni kinyume na haki za binadamu, bali ni wendawazimu uliochanganyika na upumbavu wa hali ya juu.

Nauita upumbavu kwa sababu ni afadhali ungekuwa ujinga ambao unaweza kutoka wakati mhusika anapoelimishwa. Lakini kwa kuwa yalifanywa na watu wanaojiita wasomi tena wa vyuo vikuu, basi yanakuwa ya kipumbavu maana hatujui wahusika wataenda chuo gani tena kuelimika ili wajue kuwa katika dunia tunayoishi ni vigumu watu wote kukubaliana kimawazo, hata kama mawazo hayo yanatoka kwa Rais wa nchi.

Matata na chokochoko zilizoko duniani mara nyingi huanzishwa na watu wanaojifanya kujua kila kitu, na kumbe hawajui kwamba hawajui. Na Tanzania tuna Mkapa anayejifanya kujua kila kitu na kumbe hajui impasavyo kujua. Matokeo yake ni kwamba Tanzania itaigizwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo havijawahi kuonekana popote duniani.

Nasema itakuwa vita mbaya kwa sababu karibu kila mtu Tanzania amepitia mafunzo ya kijeshi, kosa alilolifanya Nyerere akifikiri kila mtu anapokuwa mwanajeshi ni rahisi kumtawala mtu huyo. Jeshini hawaulizi maswali, bali wanatii amri.

Ni kigezo hicho ndicho kilichomfanya Nyerere aamini kuwa watanzania wakipata mafunzo ya kijeshi watakuwa na nidhamu, na itakuwa rahisi kuwatawala. Alifanikiwa kuwatawala watanzania kwa karibu miongo miwili bila ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Siyo kwamba Tanzania haikuwa na matatizo, lakini alijua nini cha kufanya yanapojitokeza tofauti na anavyofanya Mkapa ambaye anafikiri kila tatizo linatatuliwa kibabe na kutumia nguvu za dola.

Watanzania aliowatawala Nyerere ni wale wale Mkapa anaoshindwa kuwatawala, tofauti ni kwamba Nyerere aliweza kuwaibia watanzania bila wao kujua, wakati Mkapa anawaibia waziwazi. Nyerere alikuwa akigundua wananchi wamemshtukia anawaomba msamaha wa geresha wakati mkapa anamwamuru mkuu wa Polisi awashughulikie wote wanaokuwa na mawazo tofauti na chama tawala. Nao Polisi kama 'Robots' na bila kutumia ubongo wao wanawamiminia risasi za moto ndugu na dada zao watanzania na kusababisha vifo ambavyo idadi yao haitajulikana kamwe.

Serikali inasema ni watu 23 tu, wakati chama cha upinzanini CUF ambacho ndicho kilichoadhirika kwa wanachama wake kuuawa kinasema watu zaidi ya 300 waliuawa kinyama na mamia kujeruhiwa huku maelfu wakiwa wakimbizi wa kisiasa Mombasa Kenya kwa mara ya kwanza tangu Tanzania ipate uhuru. Na yote hayo yamesababishwa na utawala wa kimabavu wa dikteta Mkapa.

Kinachoshangaza na kogopesha siyo idadi ya watu waliokufa, bali tumefikia mahali ambapo Polisi wa Tanzania wanatumia bunduki zilizonunuliwa na watanzania kuwaua watanzania.

Mbaya zaidi ni kwamba karibu watanzania wote waliokufa dini yao ni ya Kiislamu jambo linalolielekeza tatizo lenyewe kuwa la kidini zaidi kuliko kisiasa. Siyo kwamba likiwa la kisiasa pekee ni rahisi kulitatua, maana sidhani Tanzania ya leo kuna mwanasiasa anayejua siasa za kutosha kulitatua.

Mkapa ni mtoto asiyekua kisiasa na siyo makosa yake. Nyerere baba yake kisiasa hakutaka akue ili awe anamnywesha maziwa ya kisiasa kila siku. Alifikiri angekuwepo mpaka azaliwe mtoto mwingine ambaye naye kama Mkapa, mpango ulikuwa kwamba asiruhusiwe kukua bali aendelee kupewa maziwa ya kisiasa sijui ingekuwa mpaka lini.

Lakini alisahau kuwa mwanadamu hawezi kuishi milele duniani, ila mbinguni au motoni ndiko watu wanakoishi milele. Mungu alipoamua kumchuku Nyerere {na sijui alimweka wapi,}Ndipo mambo yalipoanza kumharibikia Mkapa. Kama mtoto yatima kisiasa, hakujua aanzie wapi amalizie wapi.

Ninasikitika kusema kuwa mpaka sasa Mkapa amechanganyikiwa kisiasa. Wanaojifanya kumshauri ndio wanaoharibu zaidi. Inavyoonekana hatujui ni nani hasa anaeiongoza Tanzania kati ya Mboma mkuu wa majeshi, Maita mkuu wa Polisi, na Kingunge Nguoyambali Mwiru mshauri mkuu wa Mkapa. Habari kutoka vianzio vyetu zinasema kuna uvutano mkubwa kati hawa watatu kila mmoja akidai kuachiwa urithi wa Tanzania. Mboma anadai kuwa Nyerere alimwambia alinde muungano kwa nguvu zote na akiona kuna hatari ya muungano kuvunjika, Jeshi lichukue madaraka.

Kingunge naye anadai kuwa Nyerere alimwambia atumie busara yote kuhakikisha siasa zinaendeshwa bila kumwaga damu ya Watanzania. Naye mkuu wa Polisi anadai kuwa Nyerere alimwambia awafuatilie kwa karibu wanasiasa kuhakikisha kuwa hawaiuzi nchi kwa mabepari wa mataifa ya magharibi. Mkapa naye anadai kuwa Yeye ndiye aliyeachiwa nchi kuhakikisha kuwa siasa ya ujamaa haifutiki Tanzania. Ukiyaangalia madai yao, na uwe kidogo ulimfahamu Nyerere, utakubaliana nao kuwa wote wanasema ukweli.

Ni ukweli kwa sababu mwalimu alitaka kuwaona kila siku Butiama wakilalamika kwaba hili halitekelezeki kwa sababu linapingwa na lile. Yaani alihakikisha kuwa la mkapa halitekelezeki kwa sababu linapingwa na Mkuu wa Polisi. Na lile la Mkuu wa majeshi linakwamishwa na KINGUNGE NGUOYAMBALI. Wakati kila mmoja wao alipopeleka malalamiko yake Butiama ndipo Nyerere alipata nafasi ya kuwaonyesha jinsi walivyo wajinga, na inasemekana alikuwa akiwafundisha kama watoto wa Nasari.

Ndio maana wote wanamwita mwalimu. Ni kweli alikuwa mwalimu wao. Sasa Mwalimu hayupo, na wanafunzi wake wameanza kuvurunda mambo.Tayari Polisi wamewaua raia zaidi ya 50 wasiyo na hatia kwa madai kuwa walihudhuria mkutano wa kuda haki yao waliyonyanganywa na Serikali. Ni baada ya mauaji hayo ndipo Watanzania wameanza kuhoji hivi Tanzania ni ya nani hasa?

Wanajiona kama hawana haki ya kudai chochote katika nchi yao.Wakitafuta wa kulaumu wanamuona Nyerere waliyemwita BABA. Wanaona Nyerere alikosea kuwaachia urithi watu wanne tu na kuwasahau watu milioni karibu 40 kutegemea maamuzi ya watu wanne.

Matatizo yanayopikwa Tanzania sasa hivi yana michango mingi iliyochangia kuyafikisha hapo yalipo,Lakini Nyerere pamoja na kwamba ni marehemu hawezi kuepuka lawama.Aliitawala Tanzania kama mali yake, na mawazo yake ndiyo yaliyokuwa sahihi, Na hata kama aliweka Mtu, alihakikisha ni mjinga atakayeketi miguuni pake siku zote kufundishwa. Namkumbuka Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye Nyerere alifikiri ni mjinga, lakini baada ya kutawazwa kuwa Rais wa jamhuri ya muungano, alianza kufanya vitu vyake kama mwanaume anayefikiri. jambo ambalo lilimletea mikwaruzo na huyo aliyekuwa akijifanya kujua kila kitu.

Kwa sasa kuna Mkapa anayeitwa Rais wa Tanzania, Lakini nikienda Tanzania nitakutana na mzee Ali Hassan Mwinyi kwani kwangu huyo ndiye mtu aliyethubutu kuwa na mawazo huru wakati wa Nyerere kwenye uongozi wa Nyerere. Mkapa na wenzake wanatakiwa wajue kuwa sasa Nyerere hayuko, na majukumu ya kuiongoza Tanzania lazima yahusishe Watanzania wote. Kiburi kwamba wao ndio walioachiwa nchi waache.

Hata huyo wanaedai kuwa aliwaachia Tanzania haikuwa yake. Matatizo ya Zanzibar yatafutiwe uvumbuzi wa haraka unaozingatia haki na siyo ubabe kama serikali inavyojaribu kufanya. Madai ya chama cha CUF kwamba uchaguzi urudiwe na iundwe tume huru, pamoja na kubadilishwa kwa katiba yatiliwe maanani kuinusuru nchi na vita vya kidini ambavyo vinaonyesha kila dalili ya kuanza. Wakristo wasifurahi kwamba serikali ya Mkapa inawazibiti Waislamu, wajue kuwa serikali hiyo hiyo inaweza ikawageukia na wao.

Mkapa aache mara moja kuitegemea Amerika kumsadia kutatua tatizo la Tanzania kwani sera za Marekani ni kuwanyanyasa Waislamu duniani kote.Wananchi wa Tanzania wana uhuru wa kuamini dini yeyote na ikiwa Wazanzibar wengi ni waislamu sioni sababu ya wao kuadhibiwa kwa sababu ya dini wanayoiamini.

Hata kama wanataka kuuvunja muungano kwa sababu wanazozijua wao, wawe huru kufanya hivyo kwani ni kinyume kuwalazimisha kubaki kwenye muungano ambao hawaoni faida yake. Nyerere alipata sifa duniani kwa kuunganisha Tanganyika na Zanzibar, na Mkapa atapata sifa ya kutenganisha Zanzibar na Tanganyika kuepusha umwagikaji wa damu.

Kila kitu kina wakati wake. Wakati wa Nyerere ulikuwa wa kuunganisha, siyo vibaya wakati wa Mkapa ukawa ni wa kutenganisha kwa faida ya walio wengi.Kumuenzi Nyerere siyo kumwaga damu kutetea sera zake ambazo alizitetea bila kumwaga damu.

Mwisho ni vizuri Mkapa akajua kwamba yeye siyo Nyerere, na kuna vitu alivyoviweza Nyerere ambavyo yeye haviwezi. Pia asisahau kuwa kizazi alichokitawala Nyerere ni tofauti kabisa na kizazi anachokiongoza. Sura nzuri na maumbile ya Nyerere yalimsaidia kusamehewa haraka na umma, Wakati sura ya kutisha na maumbile ya ajabu ya Mkapa yanamfanya awe mtu asiyesamehewa haraka akikosa.

Tayari Mkapa ameshaukosea umma wa Watanzania kwa kuamuru Polisi wawaue zaidi ya watu hamsini huko Zanzibar, sijui itawachukua muda gani kumsamehe. Lakini kama ningekuwa Mkapa, Ningejiuzulu niombe msamaha, halafu niruhusu jeshi lichukue uongozi kwa muda, na baadaye limkabidhi Kijana Faustin Munishi madaraka.

Nafarijika na maneno haya

Utu wa mtu haupimwi na vitu; Kwani mtu ndiye anaefanya vitu, na wala vitu haviwezi kumfanya Mtu. Mtu hakamilishwi na vitu, Wala hapungui kwa kutokuwa navyo. Mtu ni Mtu hata kama hana vitu.

Ameandika Munishi

 
| http://munishi.netfirms.com |
 
<<Back  |  Home |  Gazeti La Injili | Injili2 | Nyimbo Za Munishi | Next >>